SERIKALI inaandaa miongozo ya namna ya kuvuna mikoko iliyoko kwenye maeneo ya delta ambayo inakaribia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na kuwataka wananchi waendelee kuwa na subira.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema hayo baada ya kutembelea delta ya Rufiji iliyopo mkoa wa Pwani.
Masanja alisema serikali imeandaa miongozo hiyo kwa kuwa eneo hilo la delta ni zuri lina mazalia mbalimbali ya samaki wakiwemo aina ya kamba ikiwa ni pamoja na kuepusha ukataji ovyo wa miti.
“Kipindi ambacho tutakuwa tumeruhusu uvunaji ina maana wananchi watapata faida kubwa ikiwemo uvunaji wa mazao ya misitu hususan kuvuna miti lakini wavuvi watanufaika na uvunaji wa samaki aina ya kamba,
“Eneo hili lina nusu ya mikoko yote inayohifadhiwa Tanzania wananchi waendelee kuhifadhi, ni hifadhi endelevu watu wa maliasili tuna kauli mbiu inayosema ‘Tumerithishwa, Tuwarithishe. Sisi tumerithishwa na mababu zetu tumeendelea kuhifadhi maeneo haya ili na vizazi vijavyo viendelee kurithi,” alisema.
Awali Mhifadhi Mkuu wa Wilaya ya Kibiti kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mathew Ntigwigwa alisema kutokana na ongezeko kubwa la watu kumesababisha kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kijamii ambazo zimekuwa si rafiki katika uhifadhi.
“Shughuli kubwa zaidi ni uwepo wa kilimo cha mpunga. Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika 2011 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la kilimo cha mpunga ndani ya delta 1995 ilikuwa ni hekta 3,015, mwaka 2000 hekta 3700 na mwaka 2011 eneo liliongezeka hadi kufikia hekta 8700,
“Kufikia sasa kuna uwezekano wa hekta zaidi ya 15,000 zitakuwa zimeharibiwa kutokana na kilimo cha mpunga,”alisema.
Alisema uharibifu wa mfumo mzima wa ikolojia ya bahari ya Pwani ikiwa ni pamoja na kupungua kwa miti ya mikoko, samaki na viumbe wengine baharini kutokana na ukataji mkubwa wa miti ni mojawapo ya athari za kilimo cha mpunga.
Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo alisema rasilimali za mikoko duniani zinapatikana katika nchi 118 kati ya nchi 198, Tanzania ni nchi ya tisa, nchi ya kwanza ni Nigeria.
Alisema misitu ya mikoko ya hifadhi ya delta ya Rufiji ina mfumo ikolojia wenye miti inayoota kando kando ya bahari au kwenye maingilio ya mito mikubwa baharini.
Alisema hifadhi hiyo ya mikoko ni kubwa kuliko zote katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo ina hekta 53,255 nusu ya mikoko yote Tanzania ambapo mikoko yote nchini ina hekta 115,000.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani, Ahmed Abbas alisema ili kuhifadhi eneo hilo wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi ikiwemo kilimo bora kisichoathiri eneo hilo la delta.