Utalii ni moja ya sekta nyeti zinazotegemewa na mataifa mbalimbali kukuza uchumi wa nchi. Tanzania ni miongoni mwa mataifa hayo ikiwa na utajiri wa vivutio vya utalii na maliasili.Tanzania ina aina mbalimbali za utalii na vivutio vyake kama vile hifadhi za Taifa, mbuga za wanyama, fukwe, sehemu za kihistoria, malikale na misitu.
Utalii wa misitu ni miongoni mwa maeneo muhimu na yanayokuwa kwa kasi Tanzania na duniani kwa ujumla. Huu ndiyo utalii daraja la kwanza katika viwango vya Shirika la Utalii Duniani (WTO).
Kwa Tanzania hifadhi za misitu ni eneo mojawapo lenye vivutio vya utalii vinavyotumika kwa ajili ya utalii ikolojia, utafiti, burudani za kutembea, kuendesha baiskeli, na mapumziko. Hifadhi hizi pia ni sehemu muhimu katika kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali katika jitihada za kuendeleza utalii kwenye maeneo ya misitu, ambapo mapato yanayotokana na viingilio kwenye hifadhi hizi yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.
Aidha, usimamizi wa rasilimali za malikale na maeneo ya misitu yenye vivutio vya utamaduni, unaongeza mchango katika kufikia malengo ya Serikali ya kuwa na watalii milioni tano na mapato ya dola bilioni sita kwa mwaka ifikapo 2025.
Utalii huu kwa Tanzania unasimamiwa na kuendeshwa na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS), ambapo kama wadau wa sekta ya utalii, wanaamini uhifadhi wa misitu ni muhimu katika kupeleka gurudumu la maendeleo ya utalii.
TFS unasimamia misitu ya hifadhi za mazingira asilia 20, yenye jumla ya eneo la takribani hekta 924,876.22. Kupandishwa hadhi kwa msitu kuwa hifadhi za mazingira asilia (nature forest Reserves) ni hadhi ya juu kabisa inayotambuliwa na shirika la kimataifa la uhifadhi (International Union of Conservation for Nature (IUCN), hivyo kuna jumla ya hifadhi 20 za mazingira asilia kutoka hifadhi 12 zilizokuwa na jumla ya hekta 305,600 mwaka 2015.
Hifadhi za mazingira asilia zimetengeneza mtandao mpana wenye fursa nyingi za kukuza utalii wa ndani na kwa wageni kutoka ndani na nje.